Wadau wa elimu wamekutana na kutatua changamoto mbalimbali zinazokabili shule za msingi na sekondari jana Augosti 23,2018 katika ukumbi wa Tareku wilayani Muheza.
Akisoma taarifa ya hali ya elimu wilayani hapo Afisa Elimu Sekondari Bi. Julitha Akko amesema wilaya ya Muheza ina jumla ya shule za msingi 116 zikiwemo 111 za serikali na za binafsi 5 shule za serikali zina jumla ya wanafunzi 41,981 wakiwemo wavulana 21,315 na wasichana 20,666 ambapo shule za binafsi zina wanafunzi 352 wavulana 179 wasichana 173 jumla ya wanafunzi wa binafsi na serikali ni 42,333.
Aidha kwa upande wa sekondari kuna shule 31 zikiwemo 25 za serikali na 6 za binafsi ambapo shule za serikali zina jumla ya wanafunzi 9,094 wakiwemo wavulana 4,235 na wasichana 4,859 na shule za binafsi jumla ni wanafunzi 1,437 wakiwemo wavulana 795 na wasichana 642 hivyo basi jumla ya wanafunzi kwa shule za serikali na binafsi ni wanafunzi 10,531 wakiwemo wavulana 1,030 na wasichana 5,501.
Akiendelea kusoma taarifa hiyo Bi. Julitha Akko alisema hali ya maendeleo ya elimu hasa kwa shule za serikali imekuwa ikishuka mwaka hadi mwaka ikichangiwa na utoro wa kudumu na wa rejareja kwa wanafunzi, mimba, ndoa za utotoni, mwamko duni wa wanajamii hususani wa elimu, unyanyasaji wa kijinsia, mila na desturi potofu pamoja na madawa ya kulevya.
Aliongeza kuwa kwa mwaka 2017/2018 idadi ya mimba imeongezeka sana kwa sekondari kutoka wanafunzi 24 hadi 35 pia upungufu wa vyumba vya madarasa 25 shule za msingi na 553 sekondari, matundu ya vyoo 169 sekondari na 1103 msingi, madawati 681 sekondari, walimu 356 wa msingi na walimu wa sayansi 79 sekondari.
Kwa upande wa ufaulu darasa la nne kwa mwaka 2017 wamefaulu kwa asilimia 97 darasa la saba asilimia 65.4, kidato cha pili asilimia 81, kidato cha nne asilimia 66 na kidato cha sita asilimia 100.
Aidha wadau walitoa utatuzi wa changamoto mbalimbali, Ndugu Steven Mlaguzi mwenyekiti wa kamati ya shule ya Majengo alisema, kamati za shule zishirikiane na kuwaelimisha wazazi juu ya umuhimu wa elimu, pia kuwe na mikakati ya kubaini wanaowapa mimba wanafunzi na wachukuliwe hatua stahiki na mtaala wa zamani wa kufundisha watoto wa awali miaka miwili urudishwe.
Nae Mdau mwingine Ndugu Ramadhani Nyakilama Mjumbe wa kamati ya shule alisema pesa ya elimu bure inayotolewa shuleni haitoshi hivyo basi ameiomba Serikali iongeze pesa hizo ili kukidhi mahitaji ya shule.
Vilevile Mkuu wa Wilaya ya Muheza Mhe Mwanasha Tumbo ameagiza kwamba wazazi watakaoshindwa kuwalinda na kuwasimamia watoto wao ipasavyo wachukuliwe hatua za kisheria, wazazi wa watoto wanaokwenda kwenye vigodoro na madanguro wachukuliwe hatua, pia aliagiza maafisa Maendeleo ya jamii, ustawi wa jamii na Ofisi ya OCD-Muheza washirikiane kuwaondoa watoto wanaofanyabiashara ndogondogo kwa katika stendi za mabasi na maeneo yote ya Muheza.
Wadau wa Elimu wakisikiliza kikao cha kutatua changamoto za Elimu Muheza |
|
Muheza Mjini, Bomani
Anwani ya posta: S.L.P 20 MUHEZA
Simu: 027-2977545
Simu ya Mkononi: 0746525653
Barua Pepe: ded@muhezadc.go.tz
Copyright ©2018 Muheza District Council . All rights reserved.