Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa Wilayani Muheza imerejesha fedha za wananchi kiasi cha Shilingi 12,563,000/= zilizokuwa fedha za Umoja wa wafugaji, Vicoba na Mirathi baada ya kubaini ubadhilifu uliofanywa na viongozi wa vikundi hivyo .
Hafla ya kukabidhi pesa hizo imefanyika jana tarehe 2/9/2020 katika Ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya Muheza ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya Muheza Mheshimiwa Mwanasha Tumbo.
Akisoma taarifa ya urejeshaji wa fedha hizo Mkuu wa TAKUKURU W ilaya Muheza Bi Christine Mkango amesema urejeshaji wa fedha hizo umefanyika katika mchanganuo ufuatao Chama cha Umoja wa wafugaji wa ng’ombe wa Maziwa Shilingi 6,850,000/= kikoba cha WAKUNYUMBA kimerudishiwa Shilingi 2,363,000 na Mwananchi Moshi Peter Justine fedha za mirathi Shilingi 3,400,000.
Aliendelea kuwa Serikali haitomfumbia macho mtu yeyote atakaebainika amefanya ubadhilifu kwa mtu, kikundi chama , Taasisi na mengineyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
“Tunapenda wananchi wafahamu kwamba TAKUKURU ipo imara kuwafuatilia wale wote ambao wamekuwa wakiaminiwa kupewa mamlaka ya kusimamia mali za ushirika au wananchi mmoja mmoja na matokeo yake wamekuwa sehemu ya ubadhirifu” alisema Mkuu wa TAKUKURU.
“Vile vile wakumbuke kuwa fedha hizi ni sehemu tu ya fedha ambazo wamezifanyia ubadhirifu , hatua kali dhidi ya wote watakaokaidi agizo la kurejesha fedha walizochukua zitachukuliwa kwa mujibu wa sheria ikiwa ni pamoja na kutaifisha mali za watuhumiwa kwa kushirikiana na ofisi ya Taifa ya Mashitaka” alisisitiza Bi Christine.
Pia ametoa wito kwa wananchi popote pale walipo, waendelee kutoa taarifa za wale wote wanaojihusisha na vitendo vya rushwa ili kuhakikisha kuwa hatua za kisheria zinachukuliwa dhidi ya wale wote wasiolitakia mema Taifa la Tanzania.
Aidha katika kipindi cha mwezi juni 2020 hadi tarehe 26 august 2020 jumla ya Shilingi 12,563,000.00 zimekabidhiwa kwa TAKUKURU Muheza kati ya Shilingi 24,237,000/ ambazo zilikusudiwa kurudishwa hivyo basi watuhumiwa watarejesha kiasi cha Shilingi 11,674,000 kilichobakia kwa tarehe walizokubaliana.
|
|
|
MKUU WA WILAYA MUHEZA MHE, MWANASHA TUMBO (MWENYE HIJJAB NYEUSI AKIKABIDHI FEDHA ZA MIRATHI KWA KIJANA MOSHI JUSTINE (WA KATIKATI) NI KAIMU MKURUGENZI MTENDAJI WILAYA MUHEZA AMBAE NI AFISA MIFUGO WILAYANI HUMO BW. CHRISTOPHER SIKOMBE NA WA KWANZA KULIA NI KAMANDA WA TAKUKURU MKOA WA TANGA BI SHARIFA. | MKUU WA TAKUKURU WILAYA MUHEZA BI CHRISTINE MKANGO (ALIYESIMAMA) AKISOMA TAARIFA YA UREJESHAJI WA FEDHA KWA WANANCHI. | PICHANI NI WANACHAMA NA WANAKIKUNDI WA SACCOS NA KIKOBA WALIODHURUMIWA FEDHA ZAO. |
Muheza Mjini, Bomani
Anwani ya posta: S.L.P 20 MUHEZA
Simu: 027-2977545
Simu ya Mkononi: 0746525653
Barua Pepe: ded@muhezadc.go.tz
Copyright ©2018 Muheza District Council . All rights reserved.