Halmashauri ya Wilaya ya Muheza imejipanga kikamilifu kuanza zoezi la Sensa ya Watu na Makazi linalotarajiwa kufanyika mnamo Mwezi Agosti 2022 ikiwa na lengo la kupata idadi ya watu wote katika nchi, kwa umri na jinsia, mahali wanapoishi na hali yao ya elimu, hali ya ajira, hali ya vizazi na vifo na hali ya Makazi.
Akizungumza katika kikao cha kwanza cha kamati ya Sensa Wilaya,kilichofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Muheza Mhe. Halima Abdallah Bulembo ambaye ni Mkuu wa Wilaya na Mwenyekiti wa kamati hiyo amesema akiwa katika ziara yake ya kutembelea vijiji zenye lengo la kutatua kero za wananchi amekuwa akisisitiza jamii kuhesabiwa katika zoezi la sensa.
Vile vile ameitaka jamii kuepukana na dhana potofu ya kuficha makundi maalum yaani watu wenye ulemavu wakati wa zoezi hili wawaache wahesabiwe na kuingizwa kwenye mipango ya Serikali ili waweze kupatiwa misaada wanayohitaji.
Awali akisoma taarifa ya Maandalizi ya Sensa ya watu na makazi ya Mwaka 2022 ya Wilaya ya Muheza Mratibu wa Sensa Wilaya ambaye pia ni Afisa takwimu wa Wilaya hiyo Nelson Mwankina amesema mpaka sasa kamati moja ya Wilaya, 37 za kata na kamati 126 za vijijizimeundwa kwa kuzingatia mwongozo uliotolewa na TAMISEMI.
Aliongeza kuwa maeneo ya kuhesabia yameshatengwa na kuhakikiwa na wataalam kutoka ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa kushirikiana na Viongozi wa Maeneo husika ambapo hadi kufikia tarehe 31/12/2021 kata 37, Vijiji 126 na Vitongoji 494 vimepitiwa na kuhakikiwa mipaka yake.
Aliendelea kuwa shughuli zitakazoendelea kufanyika ni uhamasishaji wa wananchi kupitia mikutano mbalimbali ngazi ya Wilaya mpaka Vitongoji pamoja na kutumia viongozi wa dini (waislam na wakristo, Walimu wakuu wa Shule za Msingi na Sekondari,Mashirika yasiyo ya kiserikali, Maafisa tarafa na Sherehe mbalimbali za kitaifa.
Kwa upande wake Mwakilishi kutoka Ofisi ya takwimu Makao Makuu DODOMA Bi. Zawadi Salehe Chanzi amezitaja baadhi ya faida za sensa kwamba husaidia kupanga maendeleo ya nchi kama vile kujenga Shule, Vituo vya kutolea huduma za afya na huduma mbalimbali jamii na kusisaidia Serikali kutatua changamoto za ardhi katika maeneo husika.
Muheza Mjini, Bomani
Anwani ya posta: S.L.P 20 MUHEZA
Simu: 027-2977545
Simu ya Mkononi: 0746525653
Barua Pepe: ded@muhezadc.go.tz
Copyright ©2018 Muheza District Council . All rights reserved.