Mapema leo tarehe 13/09/2025 Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya na Afisa Tarafa wa Tarafa ya Muheza Ndugu Ali Kijazi ameshiriki katika Maadhimisho ya Juma La Elimu ya Watu Wazima yaliyofanyika katika Viwanja vya Shule ya Msingi Kwemkabala, Kata ya Kwemkabala Wilayani Muheza.
Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya Ndugu Ali Kijazi amewatia chachu watu wazima kujitokeza kwenye vituo vya ujifunzaji vilivyopo Wilayani Muheza ili waweze kujifunza stadi mbalimbali za elimu.
“Ni wakati sasa watu wazima kujitokeza kwenye vituo vyetu kwenda kujifunza kusoma, kuandika na kuhesabu ili waweze kujiepusha madhara mbalimbali hasa ya dhuluma ya mali zao kutokana na kutokujua kusoma na kuandika” alisema Ndg. Kijazi.
Zaidi aliongeza kua, “Elimu ya Watu Wazima sio tuu Elimu ya kawaida bali kuna ujifunzaji wa ujuzi mbalimbali kama kilimo, mapishi, ufugaji kwa njia zakisasa ili kua na tija katika shughuli zetu zakujipatia kipato cha kila siku na kua na uhakika wa shughuli hizo”.
Aidha katika taarifa ya Juma la Elimu ya Watu Wazima iliyowasilishwa na idara ya Elimu Msingi na Sekondari, Halmashauri ya Wilaya ya Muheza inatekeleza programu kama MEMKWA (Mpango wa Elimu ya Msingi kwa Watoto Walioikosa), MUKEJA (Mpango wa Uwiano Kati ya Elimu na Jamii), Ufundi Stadi, ODL, QT na PC (Elimu ya Sekondari kwa Usomaji Huria.
Zaidi taarifa hio pia imeeleza takwimu za idadi ya wanafunzi/wanakisomo katika programu hizo ambapo MEMKWA inajumla ya wanafunzi 30 (Me 22 na Ke 08) katika madarasa manne kwenye Shule za msingi Mindu, Venance Mabeyo, Masuguru na Kimb, MUKEJA inajumla ya wanafunzi/wanakisomo 4646 (Me1281 na Ke 3365), huku kukiwa na Vituo viwili vya Ufundi Stadi Magila na Mkuzi na Usomaji Huria kukiwa na wanafunzi 54.
Maadhimisho hayo ya mwaka 2025 yameongozwa na kauli mbiu isemayo, “ Kukuza Kisomo katika Zama za Kidigitali kwa Maendeleo Endelevu ya Taifa Letu”, ikiwa ni juhudi za serikali kuchagiza matumizi bora ya mifumo yakidigitali katika kujifunza ili kuweza kuendana na ulimwengu wasasa wakidigitali.
Muheza Mjini, Bomani
Anwani ya posta: S.L.P 20 MUHEZA
Simu: 027-2977545
Simu ya Mkononi: 0746525653
Barua Pepe: ded@muhezadc.go.tz
Copyright ©2018 Muheza District Council . All rights reserved.