Bodi ya maji mto pangani yajenga kituo cha polisi katika kitongoji cha Kwelusanga kijiji cha Sakale kata ya Mbomole baada ya changamoto za uchimbaji madini kukithiri katika chanzo cha maji cha mto Zigi na katika hifadhi za mazingira.
Akisoma taarifa ya Ujenzi wa kituo cha polisi Agosti 21, 2018 Bi Arafa Magidi kaimu Afisa bonde la Pangani, amesema bodi ya maji bonde la mto Pangani limejenga kituo hicho kupitia mkandarasi Kumba Quality Contractors kwa gharama ya Tsh. 76,088,000/= (Milioni sabini na sita na elfu themanini na nane tu.) ambazo ni mchango wa pamoja wa Serikali ya Tanzania na wadau wa maendeleo.
Ameongeza kuwa kituo hiki kina vyumba viwili vya mahabusu, mahabusu ya wanaume na mahabusu ya wanawake, ofisi ya polisi, maliwato mbili (vyoo), na sehemu ya kupokelea malalamiko.
Akikabidhiwa kituo hicho Mkuu wa Wilaya muheza Mhe. Mhandisi Mwanasha Tumbo amesema, Kituo hiki kitawasaidia wananchi wa Sakale kuimarisha hali ya ulinzi na usalama kwa raia na mali zao, pia kuwasogezea huduma wananchi karibu kwani kituo cha awali kipo mbali sana na kijiji chao.
Pia aliwahasa wananchi wa Sakale kuendelea kuhifadhi mazingira na vyanzo vya maji kwa kuhakikisha hakuna uchimbaji wa madini utakao endelea katika kijiji hicho. “Kila mmoja awe mlinzi wa mwenzie, tuendelee kuwaondoa watu wanaoharibu mazingira” Alisema Tumbo.
Nae Kaimu Kamanda Mkuu wa Polisi Ndugu Lissu Jingi aliwashukuru wananchi na Serikali kwa ujumla kwa kujenga kituo cha polisi kwani anaamini ulinzi na usalama utaimarika sanjari na hayo aliomba kituo hicho kijengewe ghala (Amari ya kuhifadhia silaha), nyumba za kulala watumishi na huduma za kijamii ili ziweze kuwavutia watumishi watakaoletwa katika kituo hicho. Alisisitiza kuwa kazi ya ulinzi na usalama si kazi ya jeshi la polisi tu bali ni kazi ya kila mtu katika jamii kulingana na katiba ya Jamuhuri ya muungano wa Tanzania.
“Jukumu la ulinzi na usalama ni jukumu letu sote kulingana na katiba ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania” Alisema Lissu.
|
Mhe. Mwanasha Tumbo(wakatikati) akishuhudia tukio la kusaini mkataba wa makabidhiano ya kituo cha polisi kati ya Mwenyekiti wa bodi la bonde la mto Pangani Ndugu Segule Segule na Kaimu Kamanda Mkuu wa Polisi Tanga Ndugu Lissu Jingi
|
Muheza Mjini, Bomani
Anwani ya posta: S.L.P 20 MUHEZA
Simu: 027-2977545
Simu ya Mkononi: 0746525653
Barua Pepe: ded@muhezadc.go.tz
Copyright ©2018 Muheza District Council . All rights reserved.