Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Dotto Biteko, amehimiza jamii kudumisha ushirikiano na mahusiano mema kati ya mzazi, mwalimu na mwanafunzi, ili kumjenga mtoto katika ubora wa maisha yake na taaifa kwa ujumla.
Mhe Dkt. Biteko ameyasema hayo leo Septemba 30, 2024 alipokuwa akizindua kampeni ya Mtoto wa Leo Samia Kesho, ikiwa ni sehemu ya shughuli za Juma la Elimu katika wilaya ya Muheza mkoani Tanga.
Amesema ushirikiano na mahusiano hayo ni nyenzo muhimu ya kujenga mazingira bora kwa mtoto kuanzia ngazi ya familia, kwenye jumuiya za watu na shuleni anapopata elimu na maarifa ya kumfanya mtoto kuwa mwenye manufaa na tija katika ngazi zote. Mhe Dk Biteko, amewaelekeza walimu kumtazama mtoto kama kiongozi, mhandisi, daktari, mwanataaluma, kiongozi ama mzazi bora wa baadaye, na hivyo kumlinda, kumpa elimu, ujuzi, maarifa na kumlinda dhidi ya dhuluma zinazomkabili.
Pia amewaasa wazazi na walezi kuepuka matumizi majina na maneno yasiyofaa kwa watoto, kwani kwa kufanya hivyo wanawapandikizia hulka na tabia zisizoendana na uhalisia wao ili waendelee kutamani kuwa viongozi na wazazi bora wa baadaye.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe Balozi Dkt. Batilda Salha Burian, amesema kampeni hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa uboreshaji elimu, baada ya vikao vyake vya Wakuu wa Wilaya hivi karibuni.
Amesema, mazingira bora katika sekta hiyo yamechangia kupanda kwa ufaulu mkoani humo, akitoa mfano katika shule za msingi, umepanda kutoka asilimia 71 mwaka 2022 kufikia asilimia 74 (2023), wakati kwa sekondari ni kutoka asilimia 84 (2022) kufikia asilimia 89 (2023).
Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Zainab Abdallah aliyeanzisha kampeni hiyo, amesema inalenga kuleta ufanisi katika sekta ya elimu kupitia shughuli kuu za upatikanaji madawati, madarasa na kufuta sifuri na daraja la nne kwa matokeo ya kidato channe na sita wilayani humo.
Muheza Mjini, Bomani
Anwani ya posta: S.L.P 20 MUHEZA
Simu: 027-2977545
Simu ya Mkononi: 0746525653
Barua Pepe: ded@muhezadc.go.tz
Copyright ©2018 Muheza District Council . All rights reserved.