Serikali ya Wilaya ya Muheza Mkoani Tanga imesema itachukua hatua kwa wazazi ambao watashindwa kuwapeka watoto Shuleni wakiwemo wale wanaoendelea na masomo na wale wanaoanza rasmi darasa la Awali, Darasa la Kwanza na Kidato cha kwanza kwa Mwaka huu Mpya wa Masomo wa 2024 kwa kuwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ametoa fedha kwa ajili ya kuboresha Elimu.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Tawala Wilaya ya Muheza Mohamedi Mfaki kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Muheza Mhe. Juma Saidi Irando alipokuwa kwenye ziara ya ufuatiliaji wanafunzi wanaoripoti Shuleni kwa Madarasa ya Awali, la kwanza na Kidato cha Kwanza katika Shule za Msingi na Sekondari zilizopo Wilayanin humo, ambapo amewaagiza watendaji na Walimu wakuu kuhakikisha wanafuatilia wanafunzi ambao wanapaswa kuwa Shuleni.
“Napenda kutoa wito kwa wazazi wote ambao wanafahamu kabisa kwamba leo Januari 8, 2024 ni siku ya kufungua shule, na mpaka sasa watoto wao hajaripoti shuleni kwa kuwa aidha wamepelekwa kwenda kufanya kazi za ndani au kazi nyingine yoyote ile ya kuingiza kipato, niwafahamishe kwamba Mtoto hatakiwa kufanya kazi yoyote ile zaidi ya kusoma isipokuwa kusaidia kazi ndogo ndogo za nyumbani hivyo basi ikibainika kuwa mtoto wako hajaripoti Shuleni na yuko kwenye Umri wa kwenda Shule ambapo darasa la Awali ni miaka 5 na la K wanza miaka 6, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yako” alisema Katibu tawala Mfaki.
Aidha amewataka wanafunziwaliokwisha kuripoti kuachana na tabia za mtaani za kutumia madawa ya kulevya ikiwemo bangi kwani itaathiri afya zao na kushindwa kufikia ndoto za Malengo yao kwa kuwa Taifa linawategemea. Pia amewaasa wanafunzi wa kike kuacha tabia ya kushawiwa kwa kupewa zawadi za ‘Chips’ badala yake kuzingatia asomo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza Dkt Jumaa Mhina amemshukuru Dkt. Samia Suluhu Hassani kwa kutoa fedha ambazo zimesaidia kupunguza changamoto ya vyumba vya madarasa na madawati hivyo watoto wote wa Wilaya ya Muheza wanasoma kwenye Mazingira Mazuri.
Muheza Mjini, Bomani
Anwani ya posta: S.L.P 20 MUHEZA
Simu: 027-2977545
Simu ya Mkononi: 0746525653
Barua Pepe: ded@muhezadc.go.tz
Copyright ©2018 Muheza District Council . All rights reserved.