Kampuni ya Amboni Sisal Properties iliopo kata ya Kigombe wilayani Muheza mkoani Tanga imeakabidhi msaada wa fedha shilingi Milioni Sita(6,000,000/=) kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa hospitali mpya ya wilaya ya Muheza.
Risiti ya Fedha hizo ilikabidhiwa leo tarehe 27/07/2018 na mwenyekiti wa bodi ya kampuni ya Amboni Properties Neemiah Mchechu katika kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Muheza.
Fedha hizo zilikabidhiwa kwa mwenyekiti wa kamati ya uchumi,ujenzi na mazingira David Buge ambae pia ni diwani wa kata ya Misalai wilayani Muheza
Akizungumza katika kikao hicho baada ya kukabidhi risiti hiyo ya fedha Mchechu alisema kuwa kampuni ya Amboni Sisal Properties kwa kushirikiana na kampuni ya Amboni Beach Resort wametoa fedha hizo ili kusaidia ujenzi wa hospitali hiyo mpya ya wilaya ya Muheza.
Neemia alisema kuwa anatambua umuhimu wa huduma ya Afya lazima wasaidie kutoa msaada katika ujenzi wa hospitali hiyo ya wilaya ya Muheza ambayo itasaidia kuhudumia wananchi wa wilaya ya Muheza na maeneo ya jirani.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Muheza Mhandisi Mwanasha Rajabu Tumbo ambae alihamasisha ujenzi wa hospitali hiyo mpya ya wilaya katika eneo la kijiji cha Lusanga “A” alisema kuwa anashukuru kampuni ya Amboni kwa kuwezesha kusaidia fedha hizo za ujenzi wa hospitali ambao kwa sasa unaendelea kwa kasi.
Mbunge wa jimbo la Muheza Mhe. Adadi Rajabu alisema kuwa Serikali kuu imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo ya wilaya ambayo inajengwa kwa ushirikiano wa nguvu za wananchi na wadau.
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Muheza Bakari Mhando na mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Muheza Luiza Mlelwa kwa nyakati tofauti walimshukuru sana Mchechu kupitia kampuni ya Amboni kwa kukabidhi msaada huo wa fedha za ujenzi wa hospitali mpya ya wilaya ya Muheza.
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi CCM wilaya ya Muheza Mohamed Moyo na mwenyekiti wa CCM wilaya hiyo Laicky Gugu kwa nyakati tofauti walisema kuwa wataendelea kushirikiana na Mchechu kupitia kampuni ya Amboni katika kuleta maendeleo ya wilaya hiyo na kwamba chama kitamuunga mkono.
Madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Muheza walifanya kazi ya kuwasilisha taarifa za kazi mbalimbali zilizofanyika katika robo ya nne 2017/2018 katika kata zao ambapo walitoa changamato mbalimbali zinazowakabili katika kata hizo.
Muheza Mjini, Bomani
Anwani ya posta: S.L.P 20 MUHEZA
Simu: 027-2977545
Simu ya Mkononi: 0746525653
Barua Pepe: ded@muhezadc.go.tz
Copyright ©2018 Muheza District Council . All rights reserved.