MAAFISA WAANDIKISHAJI WASAIDIZI NGAZI YA KATA WATAKIWA KUZINGATIA MAFUNZO
Afisa Mwandikishaji wa Jimbo la Muheza Dkt. Jumaa Mhina amewataka Maafisa Wandikishaji Wasaidizi ngazi ya Kata wafanye kazi kwa Weledi ili waweze kusimamia zoezi la Uboreshaji wa Daftari la kudumu la
Wapiga kura linalotarajiwa kuanza Februari 13, 2025 hadi Februari 19, 2025 ikiwa ni maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka huu wa 2025.
Kauli hiyo ameitoa Alhamisi Februari 06, 2025 wakati akifungua Semina ya Mafunzo ya Uboreshaji wa Daftari la kudumu la Wapiga Kura kwa Maafisa Waandikishaji Wasaidizi ngazi ya Kata.
Semina hiyo imehusisha Mwenyekiti wa Semina, Wakufunzi kutoka Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi, Maafisa Waandikishaji Wasaidizi ngazi ya Jimbo, Afisa Uchaguzi, Afisa Ugavi, Maafisa TEHAMA wa Halmashauri na Maafisa waandikishaji wasaidizi ngazi ya kata.
Amesema Elimu hiyo wanayoipata itawawezesha kutekeleza majukumu yao ipasavyo kwani wanafundishwa namna bora ya Ujazaji wa Fomu, kutumia mfumo wa kuandikisha Wapiga Kura ( Voters Registration System - VRS) ikiwa ni pamoja na Matumizi sahihi ya vifaa vya uandikishaji Wapiga Kura.
" Ni matumaini yangu kubwa baadhi yenu mmewahi kushiriki katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya Tume ikiwemo Uboreshaji wa Daftari. Kwa kutumia Uzoefu huo na mafunzo mtakayopatiwa natarajia mtafanyakazi kwa weledi, bidii na Moyo wa kujituma ili kufanikisha zoezi hili la Kitaifa., Pia
Nawasihi kutumia uzoefu wenu kusaidia wenzenu ambao hawakuwahi kushiriki katika Uboreshaji ili waweze kutekeleza majukumu yao kikamilifu" alisema Dkt. Mhina.
Katika hotuba yake amewasisitiza Maafisa Waandikishaji Wasaidizi ngazi ya kata kuwaruhusu Mawakala wa vyama vya Siasa kuwepo kwenye vituo vya Uandikishaji ili wasaidie kuwatambua wa eneo husika bali wasiingilie utekelezaji wa Majukumu ya Waandikishaji.
Ametoa wito kwa Maafisa hao kuhakikisha wanajifunza vyema Vifaa vitakavyotumika wakati wa Uandikishaji.
Aidha amewataka kuwa na Ushirikiano kati ya Watendaji wote wa Uboreshaji, Serikali, Vyama vya Siasa na Wadau wengine wote wa Uchaguzi ili kufanikisha vyema zoezi la Uchaguzi Mkuu 2025.
Muheza Mjini, Bomani
Anwani ya posta: S.L.P 20 MUHEZA
Simu: 027-2977545
Simu ya Mkononi: 0746525653
Barua Pepe: ded@muhezadc.go.tz
Copyright ©2018 Muheza District Council . All rights reserved.