Taasisi ya Dira ya wanawake inayojishughulisha na uchakataji wa matunda, mbogamboga, utunzaji bustani na usafi wa majumbani (DIWO) imetoa mafunzo kwa wajasiriamali wilayani Muheza tarehe 3/3/2022 katika ukumbi wa CWT kwa ajili ya kuwasaidia vijana kibiashara na kujiingizia kipato.
Akizindua Mafunzo hayo, Mkurugenzi wa DIWO Bi Shamsa Danga, amesema lengo la Ziara yake ni kuhamasisha vijana wa kata ya Kicheba pamoja na wanafunzi wa Sekondari ya Kicheba 150 wenye umri kuanzia miaka 16-24 kujiunga kwenye Taasisi ili kuweza kupatiwa Mafunzo ya Ujasiriamali.
Aliendelea kuwa, Mradi huu ni wa mwaka mmoja na utafanyika kwa awamu tatu,ambapo, Awamu ya kwanza ni usindikaji wa matunda na mbogamboga, awamu ya pili ni utunzaji wa bustani na ikiwa awamu ya tatu ni usafi wa majumbani. Mafunzo haya yanahusisha ujuzi wa ufungashaji na kuongeza thamani ya bidhaa zilizochaguliwa kama vile; tomato sauce, chilli sauce, pactin, jam ya fenesi, juisi ya fenesi, viungo, matunda yaliyokaushwa, pickles, jam ya matunda, crips na pipi za maganda ya machungwa.
“Mradi huu utatekelezwa katika Kata ya Kicheba Wilayani Muheza kwasababu ya uwepo wa eneo pamoja na matunda ya aina mbalimbali, mbogamboga pamoja na viungo”. Alisema Bi Shamsa Danga.
Nae Diwani wa Kata ya Kicheba Mhe. Hamisi Mhina Mkodingo alipata nafasi ya kuzungumzia uwepo wa maeneo mbalimbali katika Kata ya Kicheba na kuahidi kutoa ushirikiano katika taasisi hiyo juu ya upatikanaji wa maeneo pamoja na malighafi zitakazotumika katika Mradi huo zitapatikana kwa wakati.
Pia Diwani wa Kibaha wa viti maalum Mhe Lidya amemshukuru Mkurugenzi wa DIWO Bi Shamsa Danga kwa jitihada za kuleta Mradi huu utakaohusisha ujenzi wa kiwanda na kuelezea kuwa ni kuunga mkono jitihada za Mhe Rais Samia Hassani Suluhu katika kazi kubwa anayoifanya. Lakini pia amethibitisha uwepo wa vifaa na jitihada zilizofanyika katika usajili wa mwanzo wa kiwanda hicho huko SIDO kinachotarajiwa kujengwa katika kata ya kicheba.
Aidha, kwa upande waVijana walioshiriki kwenye uzinduzi wa mradi huo walijitokeza na kuelezea namna walivyopokea mafunzo hayo na kuwa utawasaidia kuongeza ujuzi na kipato cha kaya.
Afisa Kilimo, Silvester Mzirai ameelezea namna ya upatikanaji wa matunda na viungo katika Wilaya ya Muheza na kuelezea changamoto mbalimbali namna matunda yanavyoharibika na kwa namna gani Mradi huu na upatikanaji wa kiwanda utapunguza changamoto hiyo.
Kijana Joyce Fadhili ambaye pia ni Mjumbe wa DIWO alitoa maelezo ya Mradi huo na ni kwa namna gani amekuwa Mjasiriamali wa kuweza kutengeneza sabuni na mafuta kwa kutumia mimea asilia kama vile parachichi na kuelezea kuwa bidhaa hizo ni nzuri na zinafaa kwa matumizi ya ngozi bila kuleta madhara ya aina yoyote.
Mwisho Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza Bw. Amiri Msuya ambaye pia ni mhamasishaji wa vijana katika Wilaya ya Muheza,ametoa shukurani na kuelezea kuwa Mradi huu umekuja katika wakati sahihi kwasababu imeenda sambamba na Miradi mingine kama Bomba la Mafuta na kuelezea kuwa itasaidia kuleta chachu ya mafanikio ya mtu mmoja mmoja na kwa Serikali kwa ujumla kwasababu itainua kipato cha wananchi kwa kutoa ajira pamoja na serikali kupitia kodi za Wananchi.
Kwa kumalizia amesema wadau wote wanakaribishwa kuwekeza na kupatiwa vibali pamoja na kupatiwa msaada wowote ambao uko ndani ya uwezo wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza.
|
||
|
||
Mkurugenzi wa taasisi ya DIWO (wa kwanza kulia) akiwa katika picha ya pamoja na diwani kata ya kicheba (wa pili kulia ) Mhe. Hamisi Mkodingo,diwani wa viti maalum Kibaha (mwenye kilemba cheusi) Mhe. Lidya Mgaya na vijana walioshiriki kwenye uzinduzi uliofanyika siku ya alhamisi tarehe 3/3/2022 katika ukumbi wa CWT- MUHEZA. |
|
Kaimu Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Muheza ambaye pia ni mhamasishaji vjana Wilaya Muheza Amiri Msuya akizungumza katika Uzinduzi wa mafunzo ya Vijana wajasiriamali. |
|
|
|
Muheza Mjini, Bomani
Anwani ya posta: S.L.P 20 MUHEZA
Simu: 027-2977545
Simu ya Mkononi: 0746525653
Barua Pepe: ded@muhezadc.go.tz
Copyright ©2018 Muheza District Council . All rights reserved.