Mkuu wa Wilaya ya Muheza Mhe. Halima Bulembo amewataka wananchi wanaoishi katika Milima ya Amani kuacha tabia ya kuvamia misitu na kuendeleza shughuli za kibinadamu kwenye vyanzo vya maji jambo ambalo linapelekea kuathiri vyanzo hivyo na badala yake amewataka kushirikiana kuvitunza kwa manufaa ya vizazi vijavyo.
Ameyasema hayo alipokuwa mgeni rasmi katika Maadhimisho ya siku ya Mazingira ambapo Kiwilaya yamemefanyika katika Kijiji cha Sakale kata ya Mbomole Tarafa ya Amani.
“Huku kwetu Sakale tarafa ya Amani kuna watu wanakuja kutembelea maeneo yetu hii ni kutokana na Mandhari mazuri iyaliyopo katika maeneo haya hivyo basi tuendelee kuyatunza, tupande miti, tutunze vyanzo vya maji, tuache kuchoma misitu, kuvamia misitu, kutupa taka hovyo na kulima katika vyanzo vya Maji ili miundombinu yetu ya maji isiharibike Mimi kama Mwakilishi wa rais wa Jamhuri ya Muungao wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan sitokubali kuwavumilia watu wachache wakoseshe watu wengine maji kwasababu tu hawataki kutunza mazingira na vyanzo vya Maji” alisema Mhe Bulembo.
Nae Meneja wa Mamlaka ya Maji Tanga Uwasa Wilaya ya Muheza Ramadhani Nyambuka amesema wamekuwa wakishirikiana na kikundi cha umoja wa wakulima uhifadhi wa Mazingira (UWAMAKIZI) kuhakikisha wanatoa elimu ya utunzaji Vyanzo vya Maji.
Aliendelea kuwa katika Maadhimisho hayo wao kama wadau wa utunzaji na uhifadhi wa mazingira wanatoa miti 1500 aina ya kuvu kuvu ambayo ni rafiki wa maji ili kulinda kingo za maji zisibomoke na kuleta tope ili kukinga chanjo chetu kikubwa cha Mabayani kisiharibike.
Awali akisoma risala katika Maadhimisho hayo Afisa Mazingira wa Wilaya SYPRIAN MSELEM amesema ndani ya Wilaya ya Muheza kuna fursa ya vivutio vya utalii vinavyotokana na utunzaji mazingira ambapo vinapatikana viumbe adimu ulimwenguni kama vile vinyonga, ua la St. Paulia, ufugaji vipepeo, maanguko ya mto zigi chemka, utalii Magila na fukwe za kigombe hivyo basi anatoa wito wa wananchi kufika katika tarafa ya Amani kujionea utalii wa kimazingira.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kikundi cha umoja wa wawakulima na uhifadhi wa mazingira (UWAMAKIZI) Twaha Mbaruku ametoa shukurani kwa Serikali na Tanga uwasa kwa namna wanavyoshirikiana kutoa elimu kwa wananchi juu ya namna bora ya utunzaji wa mazingira na vyanzo vya Maji.
Muheza Mjini, Bomani
Anwani ya posta: S.L.P 20 MUHEZA
Simu: 027-2977545
Simu ya Mkononi: 0746525653
Barua Pepe: ded@muhezadc.go.tz
Copyright ©2018 Muheza District Council . All rights reserved.