Katibu tawala wa Wilaya ya Muheza Bi. Desderia Haule amewataka wananchi kuwa na hati miliki za maeneo/ viwanja vyao ili kujiepusha na migogoro ya ardhi inayoweza kujitokeza hapo mbeleni.
Ameyasema hayo alipokuwa mgeni rasmi katika hafla ya utoaji hati miliki za maeneo ya ya viwanja vya Shaurimoyo, na Mdote iliyofanyika siku ya jumanne tarehe 13/9/2022 katika eneo la Shule ya Msingi Mdote lililopo katika kitongoji cha Majengo kata ya Majengo Wilayani Muheza.
“Ukiwa na hati una uhakika na umiliki wa eneo lako, hati hii inaondoa migogoro kati ya mtu mmoja na mwingine, ikitokea mtu amevamia eneo lako ukimpeleka kwenye vyombo vya kisheria ukionesha hati yako atakayekuja nyuma ataonekana hana uhalali na umiliki wa eneo hilo” alisema katibu tawala Muheza.
Akizitaja faida za kuwa na hati miliki za eneo au viwanja Bi Desderia amesema husaidia kupata mikopo katika taasisi za kifedha kama vile kwenye benki na taasisi nyingine binafsi zinazokopesha fedha ambazo mara nyingi huhitaji hati kama moja ya dhamana ya mkopo wa mtu,
Aliendelea kuwa hati huongeza thamani ya eneo, unapokuwa na hati miliki ya eneo lako ukitaka kulliuza eneo hilo huwezi kuliuza kwa bei ya chini kama mwenye eneo lisilo na hati.
Kwa upande wake Kamishina msaidizi wa ardhi Mkoa wa Tanga Tumaini Gwakisa amezungumzia suala la urasimishaji wa ardhi kuwa ulianza Mwaka 2010 na unatarajiwa kukamilika mnamo mwaka 2023 na mpaka kufikia siku ya leo viwanja 929 vya kata ya Majengo vimepimwa na kurasimishwa miongoni mwa viwanja hivyo 570 Vya Shaurimoyo na Mdote viwanja 359.ikiwa leo hati 131 zitatolewa kwa wananchi waliolipia na kukamilisha taratibu zote za upatikanaji wa hati.
“ Nitoe rai kwa wananchi wenzangu wa Muheza ikibainika mtu amepata Hati kwa njia ya udanganyifu tunamuondoa kwenye daftari la kumbukumbu la usajili kwa kuwa Mamlaka ya kufanya hivyo ipo kwa Mujibu wa sheria” alisema Gwakisa.
Awali akisoma taarifa ya utekelezaji wa shughuli za upimaji na urasimishaji wa ardhi katika kata hiyo Afisa Mipango Miji wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza Happiness Namponji amesema hati zitakazotolewa ni kwa ajili ya watu waliolipia gharama ya shilingi 130,000 ya upataji wa hati .
Muheza Mjini, Bomani
Anwani ya posta: S.L.P 20 MUHEZA
Simu: 027-2977545
Simu ya Mkononi: 0746525653
Barua Pepe: ded@muhezadc.go.tz
Copyright ©2018 Muheza District Council . All rights reserved.